banner

Wednesday, September 6, 2017

Pongezi za Mbowe kwa Spika Ndugai

Pongezi za Mbowe kwa Spika Ndugai

 

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe leo ametoa pongezi kwa Spika wa Bunge, Job Ndungai kwa kuunda kamati nzuri ya wabunge bila ya kujali itikadi zao na kuweza kurudisha ripoti itakayosaidia serikali.

Mbowe ameeleza hayo wakati akitoa hotuba yake katika ghafla ya kukabidhi ripoti ya kamati za bunge la Tanzania, ambazo zilichunguza biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi.

"Bunge letu likiamua kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu linayo nafasi kubwa sana ya kuisaidia serikali, kwa kuunda Kamati hizi Mhe. Spika ameisaidia serikali, nina imani Mhe. Spika na timu yake wanatambua bunge limejaa watu wenye uwezo mkubwa, 'experiences' tofauti ambao wakitumika kikamilifu wanaweza wakawa msaada mkubwa kwa taifa katika utekelezaji wa kazi za serikali", ameandika Mbowe.

Aidha, Mbowe amesema kamati hizo zimeweza kutambua madhaifu mengi katika mikataba huku akidai imekuwa kawaida ya kamati teule za bunge zinapokuwa zimetumwa kufanya majukumu yake huwa zinapeleka ripoti zilizojaa ukweli ambazo kwa bahati mbaya pengine hazitekelezwi.

"Natambua busara ya Mhe. Spika iliyompeleka mpaka aone ripoti hizi kwa unyeti wake zisisomwe tu ndani ya Bunge, lakini hata watu wengine ambao ni watendaji wakuu, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama navyo viweze kushiriki kupokea ripoti hizi. Kwa busara hizo hizo ili ripoti hizi ziweze kupata uzito wa kibunge, tuzijadili ndani ya Bunge ili wabunge sasa watoke na maazimio rasmi ambayo yatakuwa ni maelekezo ya bunge kwa serikali", amesisitiza Mbowe.

Pamoja na hayo, Mbowe ameendelea kwa kusema "kwa sababu wengi wametajwa katika ripoti hizi haki ikatendeke kwa wote, vyombo vyote vya umma vitakavyofanya kazi ya kusimamia jambo hili au maazimio yatakayokuwa ya bunge au maelekezo yeyote ya kibunge au serikali, tunaomba vikafanye kazi hii kwa haki kila mmoja apate haki inayomstahili, asionewe mtu lakini haki isiende kupindwa katika kuwakabili wahusika na changamoto zinazowahusu"

Mbali na hayo, Mbowe amempongeza Spika katika kufanya uteuzi wake katika kamati hizo  kwa kuwa umeweza kusaidia kupata kitu kilichokuwa bora , kamati hizo mbili zilikuwa zimeundwa na wabunge wa kambi zote mbili.

"Mhe. Spika alipounda Kamati teule alichanganya wabunge kutoka vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, unaona jinsi wabunge wamefanya kazi kwa pamoja siyo kwa misingi ya kiitikadi, wamefanya kazi kama viongozi, wamefanya kazi kama wawakilishi wa wananchi , wamefanya kazi kama watanzania na ripoti yao ni ya watanzania", amesisitiza Mbowe.

Kwa upande mwingine, Mbowe ameomba ushirikiano huo usiishie kwenye kamati teule tu, bali uendelee mpaka katika kulitumikia taifa kwa kuwa wote ni watanzania na nyumba wanayoijenga ni moja.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search